Katika kuadhimisha Miaka 53 ya Muungano wa Tanzania ambayo sherehe zake za kitaifa zilifanyika Dodoma, Rais John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 2,219, imeelezwa.
Tarifa ya Meja Jenerali Projest Rwegasira, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilisema wafungwa hao ambao watafaidika na msamaha huo, wataachiliwa huru.
"Ni mategemeo ya Serikali kwamba watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani," taarifa ya Jenerali Rwegasira kwa vyombo vya habari ilisema.
Msamaha huo, hata hivyo hautahusu baadhi ya makosa na taarifa ya Katibu Mkuu iliorodhesha wafungwa wafuatao kutohusika nao:
Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.
Aidha, msamaha hautawahusu wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya na wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa.
Wengine ni wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo.
Msamaha wa Rais Magufuli pia utawapitia pembeni wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali, taarifa hiyo ya Wizara ilisema.
"Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo," ilisema taarifa ya
Jenerali Rwegasira, hawatuhusika na msamaha wa Rais Magufuli.
Mbali na hao pia watu wengine ni
"Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao
walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea.
"Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo.
"Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002).
"Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.
"Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na msamaha wa Mheshimiwa Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.
"Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.
"Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu.
"Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.
"Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili.
"Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.
"Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali.
"Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 16/03/2017.
"Wafungwa warejeaji wa makosa/wafungwa waliowahi kufungwa gerezani."