Serikali imeridhia kurudisha shamba lenye ukubwa wa ekari 2,470 kwa wanaushirika wa Lokolova ililokuwa imechukua kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Mji wa viwanda na Biashara katika eneo la Lokolova wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.
Hatua hiyo imefikiwa kama moja ya fursa ya kuendeleza na kuimarisha ushirika mkoani humo ambapo vyama vingi vya ushirika vimepoteza mwelekeo na kuufanya uchumi wa mkoa wa kilimanjaro kuendelea kudorora.
Tangu mwaka 2011 serikali mkoani Kilimanjaro ilikusudia kulitaifisha shamba hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari elfu 2 ili kuepusha mgogoro wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji wa maeneo ya Lotima na Makuyuni waliokuwa wakigombania shamba hilo la Lokolova kwa ajili ya Kilimo na Malisho.
Hatimaye mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Amos Makalla katika mkutano wake wa hadhara na wanachama wa chama cha ushirika cha Lokolova pamoja na wananchi wa eneo hilo ameweka bayana hatua zilizofikiwa na kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kilichokutana Feb.12 Mwaka huu Mjini Moshi kuwa Serikali imeridhia kurudisha shamba lenye ukubwa wa ekari 2,470 kwa wanaushirika .
Mbali na ekari 2470 zilizorudishwa na serikali ya mkoa wa Kilimanjaro kwa wanaushirika wa Lokolova,serikali pia imeridhia kupokea ekari 140 zilizotolewa kwa hiari na wanaushirika hao kwa ajili kuendelea ujenzi wa soko la kimataifa la mazao ya nafaka katika eneo hilo.
Ujenzi wa Soko la Kimataifa la Mazao ya nafaka katika eneo la Lokolova unatarajiwa kuchochea fursa nyingi za kibiashara katika mpaka wa Tanzania na Kenya kutokana na kuendelea kukua kwa soko huru la Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment