Maafisa
wa serikali ya Mali wamesema sasa hakuna mateka wowote waliosalia
katika hoteli ya Radisson Blu mjini Bamako iliyokuwa imeshambulia
asubuhi na watu wenye silaha.
Waziri
wa usalama wa Mali Salif Traore ameambia kikao cha wanahabari kwamba
watu wenye silaha walioshambulia hoteli ya Radisson kwa sasa hawazuilii
mateka wowote.
Afisi
ya rais wa Mali imeandika kwenye Twitter ikishukuru maafisa wa usalama
na mataifa yaliyosaidia kukabiliana na shambulio hoteli hiyo ya
kifahari.
Watu watatu wamethibitishwa kufariki na wanajeshi wawili kujeruhiwa.
Ubelgiji imesema afisa mmoja wa serikali yake ni miongoni mwa waliouawa kwenye shambulio hilo.
Geoffrey Dieudonne alikuwa Mali kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa serikali.
Uvamizi
huo wa wanamgambo hao ulitekelezwa mapema asubuhi kwenye hoteli hiyo ya
kifahari ambayo hupendwa sana na raia wa mataifa ya nje.
Baadhi ya ripoti zilisema watu walioshambulia hoteli hiyo huenda wakafika 10.
Ufaransa
ambayo imekuwa na wanajeshi Mali tangu 2013 ilituma wanajeshi wake
kusaidiana na wanajeshi wa Mali. Aidha, polisi maalum wapatao 50
walitumwa kutoka Paris.
Kundi
la wapiganaji wa kijihadi la al-Murabitoun limedai kuhusika kwenye
shambulio hilo kupitia ujumbe kwenye akaunti ya Twitter ya kundi hilo,
kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, ingawa habari hizo
hazijathibitishwa. Kundi la Al-Murabitoun linajumuisha makundi mawili
ambayo yalijitenga kutoka kwa tawi moja la al-Qaeda eneo la Afrika
Kaskazini.
Agosti,
wapiganaji wa Kiislamu waliua watu 13, wakiwemo wafanyakazi watano wa
UN, baada ya kushikilia mateka watu katika mji wa Sevare, katikati mwa
Mali.
Ubalozi
wa Marekani mjini Bamako umeandika kwenye Twitter kwamba unafahamu
kuhusu shambulio hilo na kuwashauri wafanyakazi wake pahala salama nao
raia wawasiliane na familia.
No comments:
Post a Comment