Wanunuzi na wachuuzi wa nyama ya ng�ombe machinjio ya Vingunguti Jijini Dar es Salaam, wakiwa katika mazingira hatarishi kwa afya za binadamu. PICHA: MPIGAPICHA WETU |
Wakati
kiasi cha nyama ya ng’ombe tani 120, sawa sawa na ng’ombe 1,200
kinaliwa jijini Dar es Salaam kila siku, machinjio yanayotegemewa
yaliyopo Vingunguti manispaa ya Ilala, yamekithiri kwa uchafu, Nipashe
limegundua.
Pamoja na uchafu unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na ubovu wa
miundombinu yake, nyama inabebwa kichwani pasipo kuwapo kifaa cha kuzuia
isigusane na nywele.
Wabebaji wengine wanaiweka nyama kwenye mabega ama mgongoni wakiwa
hawajavaa vazi maalum, lakini zaidi wakitokwa jasho ‘linaloishia’ kwenye
nyama.
Nipashe imeshuhudia nyama ikibebwa katika mazingira hayo hatarishi
kwa afya ya mtumiaji, wakati nyama ikitolewa eneo la uchunaji ngozi
kupelekwa mahali pa kupima uzito, kucharangwa ama kupakiwa kwenye vyombo
vya usafiri.
Miongoni mwa wanaobeba nyama kwenye machinjio hayo wanafuga nywele
ndefu wakati wanaobeba mgongoni wanakuwa wamevaa mavazi machafu
yasiyostahili kugusana na nyama iliyo kitoweo cha walaji nchini.
Ubebabaji wa nyama kichwani unasababisha wahusika (wabebaji)
kutapakaa damu vichwani mwao, inayogandamana na nyama ambayo mwisho wa
siku inamfikia mlaji. Hali hiyo ipo kwa wanaobeba nyama begani ama
mgongoni wakiwa wamevaa nguo zisizokuwa katika ubora unaokubalika kwa
mujibu wa misingi na kanuni za afya.
Katika hali inayostaabisha ubebaji wa aina hiyo unafanyika mbele ya
macho ya wataalamu wa afya wanaokuwapo kwenye eneo hilo wakisimamia na
kutekeleza majukumu yao. Nipashe ilimtafuta msemaji kuhusu suala hilo,
Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Manispaa ya Ilala, Dk. Audifas
Sarimbo, alisema kuna sare zimewekwa kwa wafanyakazi wote wanaobeba
nyama, na kwamba wale wanaokiuka utaratibu watachukuliwa hatua kwa kuwa
kufanya hivyo kunahatarisha usalama wa nyama. Alisema kuanzia wiki ijayo
watawaondoa watu wote wanaofanya biashara nje ya jengo hilo.
NARCO YAKEMEA
Meneja Mkuu wa Narco, Dk. John Mbogoma anakemea hali hiyo akisema
ubebaji nyama unahitaji mazingira safi na usalama, vinginevyo kitoweo
hicho kitasababisha madhara ya afya kwa watumiaji wake.
MAENEO YA KUCHARANGA
Nipashe haikuishia hapo bali ilifuatilia kubaini mahali
zinapopelekwa nyama hizo, ikafika kwenye eneo linatumika kwa
kuzicharanga ambalo hata hivyo ni chafu lisilostahili kutumika kwa
shughuli hiyo.
Ni eneo lisilokuwa na sakafu badala yake nyama inawekwa na kucharangwa kwa kutumia shoka ikiwa kwenye gogo.
Kiasi cha nyama kinapokuwa kikubwa, inatandikwa mifuko ya plastiki
chini ikitumika kwa ‘kulundika’ bidhaa hiyo ikisubiri kucharangwa.
WIZI
Kukosekana kwa umakini kwa mmiliki wa nyama kumekuwa kukitoa mwanya wa wizi katika hatua tofauti hasa ya kucharanga.
“Endapo mhusika hatasimamia nyama yake wakati inacharangwa, kuna
uwezekano mkubwa wa kuibiwa,” anasema mmoja wa wafanyabiashara
aliyejitambulisha kwa jina moja la Neema.
Licha ya mazingira kuwa machafu, eneo linalotumika kwa kucharanga
nyama ni finyu lisilochochea ufanisi kwa wafanyakazi wa machinjio ama
wateja.
Ufinyu wa eneo hilo unasababisha msongamano wa watu wanaoingia
wakiwa wamevaa viatu wakikanyanga maeneo yanayotumika kwa kuhifadhi
nyama.
Hali kama hiyo ipo kwenye eneo la machinjio ambalo limetapakaa damu kiasi cha ‘kuenea’ kwenye viatu vya kila anayeingia humo.
MIFEREJI
Mchakato wa kuchuna mfugo uliochinjwa unahitaji matumizi ya maji yanayosafiri kwenye mifereji isiyotuama maji.
Lakini kwenye eneo hilo, mifereji mingi imeziba hivyo kusababisha
maji yaliyochanganyika na damu kutuama, hali inayotishia magonjwa ya
mlipuko na harufu katika eneo hilo. James Charles ni mnunuzi wa nyama
kwenye machinjio hayo, anathibitisha kuwa mazingira yaliyopo si rafiki
kwa afya za wadau wakiwamo wachinjaji, watoa huduma na wanunuzi.
Anasema kutokana na hali hiyo, ipo haja kwa serikali kuweka mkakati
madhubuti utakaosababisha kudhibiti udhaifu uliopo kwenye miundombinu
ya machinjio hayo ili ikidhi vigezo, misingi na kanuni za afya.
MNADANI HALI TETE
Kama ilivyo kwa machinjio ya Vingunguti, eneo la mnada wa ng’ombe
huko Ruvu linalotumika kwa kuhifadhi na kuuza mifugo hiyo, linakabiliwa
na miundombinu mibovu licha ya tozo za ushuru zinazokusanywa kutoka kwa
wafanyabiashara.
WASAFIRISHAJI
Pamoja na nyama inayochinjwa kuwa kwenye mazingira machafu, lakini
usafirishaji wa ng’ombe kutoka mikoa mbalimbali unachangia kuidhoofisha
nyama baada ya kuchinjwa. Miongoni mwa vyanzo vinavyochangia hali hiyo
ni ukosefu wa malisho na maji kwa mifugo inayosafirishwa kati ya siku
tatu hadi tano kwa kutumia magari, bila kula wala kunywa. Mmoja wa
wasafirishaji wa ngombe, Omary Kalimba, anathibitisha hali hiyo na
kuongeza kuwa msongamano wa ng’ombe wengi kwenye gari unachangia pia
kuathiri afya na ubora wa nyama. “Mara nyingi tunaposafirisha idadi
kubwa kwenye lori, ng’ombe wanasumbuka kwa msongamano na inapotokea
wengine kuanguka hasa kutokana na dereva kushika breki za ghafla,
wanaweza kukanyagwa hadi kufa,” anasema.
MACHINJIO YA RUVU
Nipashe ilifika katika eneo la Ruvu wilayani Bagamoyo palipo na
mradi wa machinjio ya kisasa uliopangwa kugharimu Shilingi bilioni tisa.
Hata hivyo mradi huo ulisitishwa mwaka juzi kwa kile kilichoelezwa kuwa
ni mkandarasi aliyeshinda zabuni hiyo, Suma JKT kukiuka makubaliano ya
mkataba.
Mradi huo ulitarajiwa kuwezesha kuchinja ng’ombe 1,000, mbuzi 1,500
huku ukitoa ajira zaidi ya 200. Kushindwa kukamilika kwa mradi huo
kumesababishia kuanzishwa kwa machinjio ya mbuzi ambayo yapo eneo
Mazizini, njia ya kwenda Kitonga huku Ruvu wakiendelea wakichinja kwa
njia za kiasili na kuning’iniza nyama juu ya miti. Kwa hivi sasa eneo la
mradi huo halina miundombinu zaidi ya kamba zilizotundikwa kwenye miti,
zikitumiwa na wachinjaji wa mbuzi kwa njia za asili wanalipia ushuru wa
Sh 500 kwa kila mbuzi anayechinjwa.
Pia eneo hilo ambalo lipo umbali wa takribani mita 570 kutoka
barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda Morogoro ni chafu kutokana na
kutofanyiwa usafi baada ya kuchinja.
Nipashe ilielezwa na vyanzo tofauti kuwa kutokana na eneo hilo kuwa
mbali na barabara, wachinjaji wanalazimika kubeba maji lita 10 za ujazo
kwa ajili kuoshea nyama na utumbo lakini hayatoshi.
Baadhi ya wenyeji wa eneo hilo wanaelezea kuishi katika mazingira magumu huku serikali ikiacha kuchukua hatua.
“Sisi tukizungumzia jambo hili tunapewa vitisho, hivyo hii hali
tumeizoea, mvua ikinyesha hata kula tunashindwa na huu uchafu wote
unaouona unaenea hadi kwenye mto Ruvu,” anasema mkazi wa Ruvu anayeomba
jina lake lisitajwe kwa sababu za kiusalama.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ruvu, Kambona Kwalo, anasema
hakuna haja kwa wakazi hao kuilalamikia hali hiyo kwa vile eneo hilo
lilitengwa mahususi kwa ajili ya machinjio. Kwalo anasema mpango wa
serikali wa kujenga machinjio hayo bado upo na kwamba wanavijiji
wanapata taarifa za mchakato wake kupitia vikao vyao.
Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco) inachinja ng’ombe kati ya
watatu hadi watano kwa siku na kuuza nyama kwa wananchi, lakini hawana
machinjio ya kisasa.
Machinjio yaliyopo Narco yaliezuliwa mabati kutokana na upepo mkali
uliowahi kutokea kwenye eneo hilo, hivyo kuwalazimu kujenga ya muda.
Meneja Mkuu wa Narco, Dk. John Mbogoma, anasema sekta ya nyama
inahitaji uimarishaji wa miundombinu, kuwapo kwa viwanda na mazingira
mazuri ya biashara.
Anasema serikali ilibuni mradi wa Ruvu kuwa machinjio ya kisasa
lakini Suma JKT hawakufanya vizuri hivyo kusitishiwa mkataba wao. Hali
hiyo ilifikia baada ya majadiliano ya muda mrefu ikiwamo shauri
lilihitimishwa kwa Suma JKT kuamriwa kulipa Sh. milioni 800 kutokana na
kusitishiwa mkataba huo. Dk. Mbogoma anasema kwa sasa wapo katika
mchakato wa kumpata mzabuni mwingine ili kuendeleza mradi huo na tayari
kampuni kadhaa za ndani zimeomba zabuni hiyo. “Tunaendelea na mazungumzo
na ifikapo Desemba tunatarajia kuwa ujenzi utaanza,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk. Mbogoma, mradi huo utagharimu Dola za Marekani milioni 20 (sawa na takribani Sh bilioni 42).
Anasema mradi wa Ruvu ukikamilika, machinjio ya Vingunguti
yatageuzwa kuwa kituo cha usambazaji nyama zinazotokea eneo la mradi
(Ruvu).
NYAMA TANI 120 ZATAFUNWA DAR
Dk. Mbogoma anasema takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa nyama yenye
uzito wa tani 120 za nyama (sawa ng’ombe 1,200) inaliwa jijini Dar es
Salaam kila siku, hivyo kuwa moja ya sababu ya kutoa kipaumbele kwa
sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Dk. Mbogoma, kama kutakuwa na mikakati mzuri kwa
sekta hiyo, uzalishaji wake utaongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi kwa
kiwango kikubwa.
Anasema licha ya kuchinja mifugo, Tanzania inasafirisha kiasi cha
ng’ombe 300,000 kwenda Kenya ambao baada ya kuchinjwa, nyama inarejeshwa
nchini na kuuzwa kwenye maduka makubwa maarufu kama Super markets.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment