MGOMBEA urais wa CCM, Dkt. John Magufuli, amewataka wakazi wa Jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro, kutompigia kura mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Alisema kama hawataki kumpigia kura mgombea ubunge wa CCM, Bw. Innocent Shirima, basi wanaweza kumchagua Mwenyekiti wa TLP anayegombea ubunge jimboni humo, Augustino Mrema.
Dkt. Magufuli aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Himo akisema Mbatia amekuwa akimnyima amani Mrema mbali ya kuondoka NCCR-Mageuzi, lakini bado amekuwa akimfuata jimboni; hivyo wamnyime kura kwani hafai kuwaongoza.
"Kama hamtaki kumchagua mgombea ubunge wa CCM, mchagueni Mrema ambaye mara nyingi amekuwa akiwatetea bungeni...simaanishimsimchague Shirima, huyu ndiye ninayemhitaji ili niweze kumtumia katika harakati za maendeleo ya jimbo hili," alisema.
Aliongeza kuwa, Mbatia ameshindwa kukijenga chama chake badala yake amekuwa akijivika vyeo ndani ya UKAWA, hivi sasa amekuwa msemaji wa CHADEMA na kukiacha chama chake.
Aliufananisha UKAWA na magari manne ambayo yote ni mabomu yanayoshindana na gari jipya CCM na kuwataka wananchi kutambuakuwa, yeye ndiye Rais wa Awamu ya Tano, hivyo Oktoba 25, mwaka huu, wasihangaike kuwapigia kura wapinzani.
Mrema na Dkt. Magufuli uso kwa uso
Katika hatua nyingine, Dkt. Magufuli baada ya kumaliza mkutano Jimbo la Vunjo, akiwa njiani kwenda Wilaya ya Mwanga, msafara wake ulisimamishwa njiani na Mrema ambaye aliwasihi wakazi wa Himo wamchague Dkt. Magufuli kuwa rais wao.
"Dkt. Magufuli ni mchapakazi na ndiye rais wetu, hakikisheni Oktoba 25, mwaka huu, mnampigia kura nyingi...amefanya mengi ndani ya CCM kwani amejenga barabara nyingi katika wilaya hii," alisema.
Jimbo la Rombo
Awali, Dkt. Magufuli akiwa wilayaji Rombo, aliwataka wakazi wa Tarakea kumtafutia kazi ya kufanya mgombea ubunge wa CHADEMA, Joseph Selasini kwani hatoshi kuwa mbunge wao, ameshindwa kazi.
Alisema Selasini hafai kuwa mbunge kwani miaka yote aliyokaa bungeni alikuwa akitoka nje wakati Bunge likijadili matatizo ya Watanzania.
Dkt. Magufuli aliyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Tarakea Mpakani akiwataka wananchi wafanye mabadiliko ya mbungena kumchagua wa CCM badala ya kuendelea kumsikiliza Freeman Mbowe ambaye naye ameshindwa kuwasaidia wananchi.
Wilaya ya Mwanga
Akiwa katika Wilaya ya Mwanga, Dkt. Magufuli alisisitiza kuwa yeye ni tingatinga ambalo kazi yake ni kufanya kazi; hivyo atahakikisha muda wote anawatumikia Watanzania ili aweze kuleta mabadiliko nchini.
"Nawaomba mnichagulie wabunge na madiwani wote wa CCM ili niweze kuwatumia kuharakisha maendeleo yenu...ukimpenda Magufuli lazima upende na funguo, mimi ndiye ninayetosha kuwa rais," alisema.
No comments:
Post a Comment