Tuesday, November 24, 2015

Uwakilishi huu wa mwananchi ni wa mashaka

HABARI kwamba wabunge wana mpango wa kugomea Sh milioni 90 zilizotengwa kwa ajili ya kununua magari aina ya Toyota Land Cruiser (hardtop) kama vitendea kazi, yanatia shaka kama kweli wako tayari kumsaidia Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli ambaye kaulimbiu yake ni ‘Hapa Kazi Tu.’
Tafsiri rahisi ya ‘Hapa Kazi Tu’ naichukulia kama ni kuona kila mmoja anawajibika ipasavyo ili kuiletea nchi maendeleo, kuondoa ubinafsi uliokithiri kwa watendaji wa mashirika ya umma, taasisi za serikali na kampuni binafsi na pia kufanya utumishi uliotukuka kwa wananchi. Akizindua Bunge mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, Rais Magufuli, hakusita kuonesha kukerwa na baadhi ya matumizi mabaya ya rasilimali za nchi kwa watendaji wa serikali.
Alitolea mfano wa Sh bilioni 356 zilizotumika kwa safari za nje katika mwaka wa fedha wa 2013/14 na 2014/15 pekee. Mbali na mfano huu wa matumizi mabaya ya fedha za serikali, kuna maeneo mengi tu ambayo angekuwa na nafasi ya kutosha, yangeweza kuanikwa kwa wabunge. Hata hivyo, Rais Magufuli aliomba wananchi pamoja na wabunge wenyewe kumsaidia katika hili.
Akawakumbusha wabunge hali halisi ya kipato cha wananchi kwa jinsi walivyoiona wakati wa kampeni na matarajio yao makubwa hadi kuwachagua wabunge na yeye mwenyewe kama rais. Wakati tukifikiria maeneo ya kupunguza matumizi, tayari wabunge wamekuja na mpya; kwamba hawako tayari kupewa Sh milioni 90 ili kununulia magari kwa ajili kutendea kazi zao za kila siku!
Ikumbukwe katika kuonesha kukerwa na haya matumizi makubwa, Rais Magufuli alihoji katika hotuba yake hiyo, kuwa inakuwaje mhandisi katika wizara anayewajibika kukagua miradi katika maeneo ya vijiji, anapewa Toyota Land Cruiser (hardtop) badala ya kupewa Toyota pick up inayoendana na kazi yake?
                                                

Mtazamo wangu ni kwamba wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, hawahitaji magari makubwa ambayo ni ya anasa, tena kila baada ya miaka mitano (kwa wale wanaorejea bungeni).
Hawa ndio wasimamizi wakubwa wa miradi serikalini wanaohitaji Toyota pick up ili washughulikie matatizo ya wananchi kwa ukaribu na kama kweli wanajua umaskini wa Watanzania, wangefikiria magari ya bei rahisi zaidi yenye uwezo uleule ambayo yapo. Wapo wanaosema kama kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya Rais Jakaya Kikwete walipewa Sh miloni 60, awamu yake ya pili, dau likaongezwa hadi Sh milioni 90, hivyo hivi sasa wanataka waongezewe iwe kiasi cha Sh milioni 120 au 130.
Nimevutiwa na msimamo wa Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu ambaye mbali na kukemea wenzake kwa kujikita zaidi kwenye kujilimbikizia mali badala ya kuwatumikia wananchi, yuko tayari hata kuacha posho ya vikao (Sh 300,000) ya kila siku kwani anaamini mshahara wake unamtosha. Huo pia ndio msimamo wa Zitto Kabwe ambaye amekuwa hachukui posho hizo.
Sina uhakika na msaada wabunge watakaompa Rais Magufuli kwani hata kabla ya wiki haijasha baada ya kuombwa kumsaidia katika kupunguza matumizi ya Serikali, tayari wameonesha nia ya kupanua wigo wa masurufu yao! Ni kawaida kuona wanasiasa wakipambana kuingia bungeni kwa kisingizio cha kuwa na uchungu na matatizo ya wananchi, ‘ndio maana wako tayari kutoa chochote’ ili wawasaidie wananchi katika matatizo yao.
Kwangu mimi, nalichukulia suala la kuwepo kwa marupupu kibao yakiwamo hata ya kiinua mgongo ambacho nacho ni mamilioni ya fedha ikilinganishwa na mtumishi wa serikali aliyeitumikia kwa uaminifu nchi yake kwa zaidi ya miaka 30, ni kichocheo cha wabinafsi kukimbilia siasa. Ninachotaka kusema ni kwamba tunachoshuhudia wakati wa uchaguzi kumbe ni mpambano wa ‘ulaji’ kuliko ‘kutumikia wananchi’.
Nadhani, ili kumsaidia Rais Magufuli, ni vema kila mmoja wetu kuanzia mwananchi wa kawaida, watendaji na watumishi wa umma, taasisi na sekta binafsi tukaondoa ubinafsi na kujiandaa kuweka maslahi ya taifa mbele.
Kama kila mmoja wetu anaijua Tanzania kama ninavyoijua mimi, ni wakati wa kuacha porojo na unafiki. Tuwe wakweli kuisaidia jamii ya Watanzania kuondokana na umaskini uliokithiri badala ya uwakilishi kuwa mradi wa kuwafaidisha wachache

No comments:

MUSIC